

MJUE HASSAN MOROWA
Ahlan! Mimi ni Hassan Morowa
DHAMIRA YA WAZI
Naomba kuwasikiliza watu wangu kwa makini, ili kwa pamoja tuweze kuimiliki na kuitumia ardhi yetu tajiri, mila na tamaduni zetu za kuigwa na utenda kazi wetu ili tuifanye Tana River makao makuu ya kuilisha Kenya nzima.
Tukishirikiana nawe naahidi kuubadilisha mustakabali wa Tana River ili kila familia ifaidike.
Sauti Yako. Chagua Lako. Ndio Ahadi Yetu.
UJUMBE KUTOKA KWANGU

Mimi ndiye Hassan Morowa. Nilizaliwa na kukulia Tana Delta. Niligombea kiti cha Ugavana 2022, na nikawa nambari 6 kwa jumla ya wote waliowania kiti hicho. Katika jamii ya Wapokomo (ambayo mimi ni mmoja wao), niliibuka wa pili kati ya wagombeaji tisa. Kundi la Wapokomo ndilo kubwa zaidi kwa idadi ya kura. Najitosa tena uwanjani mwaka wa 2027, nikiwa nimesoma mengi zaidi, nikaongeza hekima,na kurekebisha nilipokosea, tayari kuunganisha jumuiya zote-Pokomo, Orma, Wardei na kwingineko. Ni muhimu kukumbusha umma kwamba aliyeibuka mshindi 2022 keshamaliza muhula wake wa pili kwa hiyo haruhusiki tena kuwania kiti cha Ugavana 2027. Kwa hali hii, naona tuna nafasi nzuri ya kuibuka mshindi mara hii. Huu ni wakati wa kuchagua uongozi unaosikiliza, unaojumuisha kila mtu na kuleta maendeleo ya uhakika bila ubaguzi.
Sauti Yako. Chaguo Lako. Ndio Ahadi Yetu.
ASLI YA HASSAN MOROWA
Hassan Morowa alizaliwa katika kijiji cha Nduru eneo la Chara, Tana Delta. Ni kitinda mimba wa familia ya marehemu Alhaj Muhammad Ali Hiribae na Mama Bona Rhoka. Baba yake alisoma darasa moja na Sheikh Omar Dima kutoka kijiji cha Kilindini kule Kinakomba. Walipo hitimu, mwalimu wao mkuu wa Riyadha Lamu, Habib Swaleh Jamalulayl alimtuma Sheikh Omar Dima kwao Kinakomba na Alhaj Muhammad Ali akamtuma sehemu za Chara. Huu ni wakati ambao Wapokomo walikuwa wakifuata imani za jadi. Wote wawili waling'ang'ana mpaka wakaweza kuueneza uislamu Tana River upande wa Wapokomo na Waorma. Hassan Morowa alikulia katika mazingira haya na maadili yake ya uaminifu, heshima na upendo yanatokana na malezi haya aliyoyapata. Leo hii, anaendeleza maadili hayo kama baba wa watoto wanne-Morowa, Abiyo, Al-Amin, na Zeynab Bona. Ni kiongozi anayependa haki, umoja na maendeleo kwa kila mkaazi anayeamiliana naye.
UTENDA KAZI WAKE
Hassan Morowa ni mfanyabiashara mashuhuri jijini Nairobi. Dira zinampa nafasi kubwa ya yeye kunyakua kiti cha Ugavana wa Kaunti ya Tana River mnamo 2027. Akiwa mwanauchumi kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, alijiunga na tasnia ya benki kwa karibu miongo miwili. Safari hii aliianza Habib (K) Finance, kisha akaenda Habib Bank AG Zurich, First American Bank (baadaye ikawa Commercial Bank of Africa) na Cooperative Bank of Kenya alipoamua kustaafu na kuanza biashara zake mwenyewe. Kwa sasa biashara zake zimejikita katika sekta ya Afya, Studio na teknologia. Hassan amewalea na kuwatia moyo makumi ya watu ambao sasa wamehitimu na kuanza kuendeleza biashara zao katika kaunti mbalimbali zikiwemo Tana River, Mombasa, Kwale na Nairobi.
Sauti Yako. Chaguo Lako. Ndio Ahadi Yetu.

